KAIMU MGANGA MKUU WA MKOA WA MTWARA BI: HERIETH KIPUYO AFUNGUA MAFUNZO YA VITENDO YA UNYUNYIZIAJI WA VIUADUDU VYA KIBAIOLOJIA KWENYE MAZALIA YA MBU KWA WAKUFUNZI NGAZI ZA MIKOA NA HALMASHAURI KANDA YA KUSINI
Posted on: January 16th, 2026Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bi: Heriet Kipuyo amefungua mafunzo ya vitendo ya unyunyiziaji wa Viuadudu vya kibaiolojia, katika maeneo yenye mazalia ya mbu kwa wakufunzi kutoka Kanda ya kusini. Mafunzo hayo yanafanyikia katika ukumbi wa Veta Manispaa ya Mtwara Mikindani kuanzia tarehe 15 – 16 Januari, 2026 na yanahusisha Waratibu wa malaria wa Mikoa na Halmashauri, Maafisa kutoka kitengo cha mazingira na taka ngumu, Wadhibiti wa Wadudu dhurifu, pamoja na Waratibu wa elimu ya Afya kwa umma kutoka katika Halmashauri zote za Mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi.
Lengo la mafunzo hayo hayo ni kuhakikisha kuwa wataalam ngazi za Mikoa na Halmashauri wanajengewa uwezo ili kuwawezesha kutekeleza afua ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwa ufanisi na kuleta matokeo. Mafunzo hayo yanahusisha elimu ya darasani na mafunzo kwa vitendo.
Bi. Herieth amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia elimu watakayoipata katika kuleta tija ya utendaji kazi kwenye maeneo yao hususani katika kudhibiti mbu waenezao malaria ili kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria katika Mikoa yao.
Aidha, amesistiza kuwa kila Halmashauri iandae mpango kazi wake ambao utakuwa endelevu utakaohusisha afua mbalimbali za kupamba na ugonjwa wa malaria ndani ya Halmashauri na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake kila mwezi katika ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wake kwa ajili ya ufuatiliaji.

Bi: Herieth ametoa wito huo Januari 15, 2026 alipokuwa akiongea katika kikao cha ufunguzi na washiriki hao, ambapo pia amewasisitiza washiriki kwenda kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa Malaria katika Halmashauri zao na umuhimu wa wananchi kusafisha Mazingira yanayozunguka maeneo yao.
Mpango wa unyunyiziaji wa Viuadudu kwenye mazalia ya mbu unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya unalenga kupunguza mbu waenezao malaria na hatimaye kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini ili kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo mwaka 2030.