Girl in a jacket

MINISTRY OF HEALTH

National Malaria Control Programme (NMCP)

Girl in a jacket

KIKAO CHA WATAALAMU WASHAURI WA AFUA ZA UDHIBITI WA WADUDU DHURIFU WAENEZAO MAGONJWA KINAFANYIKA MKOANI DAR ES SALAAM

Posted on: February 17th, 2026

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kwa kushirikiana na Swiss TPH kupitia mradi wa TEMT,  inaendesha Kikao cha wataalamu washauri wa afua za udhibiti wa wadudu dhurifu waenezao magonjwa, mkazo ukiwa katika udhibiti wa mbu waenezao Malaria. Kikao hicho ambacho ni cha robo ya kwanza kwa mwaka 2026, kinafanyika Mkoani Dar es Salaam tarehe 16 hadi 18, Februari, 2026 na kinashirikisha Wataalam wabobezi wa afua za udhibiti wa wadudu dhurifu waenezao magonjwa na wametoka katika Taasisi za Utafiti na Vyuo Vikuu mbalimbali hapa nchini, Wizara ya Afya, Shirika la Afya Duniani, Taasisi ya Marasis wa Afrika Katika mapambano dhidi ya Malaria (ALMA), Wadau watekelezaji, Asasi za Kijamiii na Washauri elekezi wa masuala ya udhibiti wa wadudu dhurifu.

Kikao hiki kinapitia na kujadili masuala mbalimbali ya kitaalam yanayohusu utekelezaji wa afua za udhibiti wa mbu waenezao malaria hapa inchini, hususan matumizi ya afua ya vyandarua vyenye dawa, unyunyiziaji wa viuadudu vya Kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu, utunzaji wa mazingira, ufuatiliaji wa mbu na tabia zao ikiwemo usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vinavyotumika na kudhibiti mbu hao, na viashiria vingine muhimu katika kupima matokeo ya utekelezaji. 

Aidha kikao kinajadili kwa kina juu ya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa malaria wa mwaka 2021-2025 pamoja na viashiria muhimu vya kipaumbele kwa lengo la kuandaa Mpango Mkakati mpya wa Malaria wa mwaka 2026-2030.

Kikao hiki kinatarajiwa kutoka na maazimio muhimu ambayo yatasaidia katika kutoa mwelekeo mpya kwa ajili ya kuzingatiwa kwenye Mpango Mkakati mpya wa malaria ili kuweza kufikia lengo la kutokomeza malaria hapa nchini ifikapo mwaka 2030.

}