KIKAO KAZI CHA KUHUISHA MWONGOZO WA KITAIFA WA VIPIMO VYA MALARIA CHAFANYIKA MKOANI MOROGORO
Posted on: August 12th, 2026Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) kwa kushirikiana Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI (OWM-TAMISEMI), Wataalamu mbalimbali wa afya, Washauri elekezi pamoja na Wadau wamekutana katika kikao kazi mkoani Morogoro kwa ajili ya kupitia na kuhuisha Mwongozo wa Kitaifa wa vipimo vya malaria wa mwaka 2026. Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 10 hadi 12 Agosti 2026.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi hicho, Mkuu wa Kitengo cha uchunguzi na matibabu ya Malaria kutoka NMCP, Dkt. Abdallah Lusasi amesema kuwa lengo la kuandaa na kuhuisha Mwongozo huo ni kuhakikisha kuwa huduma za vipimo vya malaria zinatolewa kwa viwango vilivyowekwa, kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi na kanuni za utekelezaji ili kutoa huduma bora za utambuzi wa malaria hapa nchini katika ngazi zote.
Maeneo muhimu yaliyomo katika mwongozo huo ni pamoja na; Uchunguzi na utambuzi wa vimelea vya malaria, mfumo wa ubora wa uchunguzi wa Malaria kwa kutumia Hadubini, Kipimo cha Haraka cha Utambuzi wa Malaria (mRDT) , mfumo wa usimamizi wa ubora, uhakiki wa majibu ya vipimo vya vya malaria, tathmini ya umahiri kwa wataalamu wa maabara kwenye kipimo cha uthibiti ubora wa nje wa vipimo vya malaria (EQA), usimamizi shirikishi, upimaji na utambuzi wa malaria katika Vituo vya kutolea huduma vya Binafsi na Maabara binafsi zinazojitegemea, utambuzi wa vimelea vya malaria kwa mbinu za kimaabara na kijenetiki (Molecular Diagnostics), utambuzi wa vimelea vya malaria unaosaidiwa na teknolojia za kidijitali (AI), usimamizi wa taarifa, ufuatiliaji na tathmini.
Afua ya vipimo na utambuzi wa vimelea vya malaria ni miongini mwa afua muhimu katika mkakati mkuu wa uchunguzi na matibabu sahihi ya malaria. Mikakati mingine ni udhibiti wa mbu waenezao malaria kwa njia mbalimbali, ufuatiliaji na tathmini ya ugonjwa wa malaria, elimu, hamasa na ushirikishwaji jamii, pamoja na upatikanaji na usambazaji wa dawa na bidhaa za malaria katika ngazi zote. Mikakati yote hii inatekelezwa ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.