KIKAO KAZI CHA KUPITIA NA KUANDAA MWONGOZO MPYA WA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MALARIA CHAFANYIKA MKOANI MOROGORO
Posted on: June 16th, 2026Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) kwa kushirikiana na Wataalamu mbalimbali, Washauri elekezi pamoja na Wadau wamekutana mkoani Morogoro leo tarehe 15 Juni, 2026 kwa ajili ya kupitia na kuandaa Mwongozo wa Uchunguzi na Matibabu ya malaria kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa mwongozo huo, Mkuu wa Kitengo cha uchunguzi na matibabu ya Malaria kutoka NMCP, Dk. Abdallah Lusasi amesema kuwa lengo la kuandaa Mwongozo huo ni kuhakikisha kuwa huduma za uchunguzi na matibabu ya malaria zinatolewa kwa viwango na taratibu zinazofanana kulingana na kanuni zinazotakiwa na kwa weledi katika ngazi zote za huduma hapa nchini. Aidha, Dr. Lusasi amesisitiza kuwa Mwongozo huo, utakapokamilika utawezesha kuboresha huduma za malaria kwa kuhakikisha kuwa wagonjwa wanachunguzwa na kutibiwa kwa usahihi. Maeneo muhimu yaliyomo katika mwongozo huo ni pamoja na uchunguzi wa vimelea vya malaria kwa kutumia kipimo cha haraka (mRDT) pamoja na Hadubini, matibabu ya malaria isiyokali na matibabu ya malaria kali, pamoja na orodha yaa dawa zinazotumika, uchunguzi na matibabu ya malaria ngazi ya jamii, tiba kinga ya malaria kwa wajawazito, wanafunzi wa shule za msingi, watoto chini ya mwaka mmoja wanapohudhuria kliniki, na wanajamii katika maeneo yenye kiwangi cha juu cha maambukizi ya malaria hususan maeneo yenye mvua za vipindi.
Maeneo mengine ni kuzuia usugu wa vimelea vya malaria dhidi ya dawa kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya dawa za malaria, chanjo ya malaria, ufuatiliaji na usimamizi wa huduma za malaria katika vituo vya afya vya sekta binafsi pamoja na kutumia ubunifu katika utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya malaria.
Mkakati wa uchunguzi na matibabu sahihi ya malaria ni miongoni mwa mikakati mikuu ya kupambana na malaria hapa nchini, ikiwemo pia udhibiti wa mbu waenezao malaria kwa njia mbalimbali, ufuatiliaji na tathmini ya ugonjwa wa malaria, elimu, hamasa na ushirikishwaji jamii, pamoja na upatikanaji na usambazaji wa dawa na bidhaa za malaria katika ngazi zote.