MAAMBUKIZI YA MALARIA YAPUNGUA KWA ASILIMIA 45 NCHINI
Posted on: April 24th, 2025
Na WAF – Dodoma
Takwimu zinaonesha kuwa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini yameendelea kupungua katika kipindi cha miaka saba kwa asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Aprili 25, 2025, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya Malaria duniani ambayo huadhimishwa tarehe 25 Aprili, 2025 kila mwaka duniani kote.
Waziri Mhagama amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na juhudi za Serikali katika kutekeleza mikakati na afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo na kuwezesha kupungua kwa idadi ya wagonjwa waliothibitika kuwa na Malaria kwa asilimia 45 kutoka wagonjwa milioni 6 mwaka 2020 hadi kufikia milioni 3.3 mwaka 2024.
“Serikali imesaidia kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaolazwa kutokana na Malaria kwa asilimia 33 kutoka wagonjwa 306,633 mwaka 2020 hadi kufikia wagonjwa 206,453 mwaka 2024,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama ameongeza kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na Malaria imepungua kwa asilimia 39 kutoka vifo 2460 mwaka 2020 hadi kufikia vifo 1503 mwaka 2024.
Hata hivyo, Waziri Mhagama ametaja Mkoa wa Tabora kuwa kinara wa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini kwa asilimia 23 ukifuatiwa na mkoa wa Mtwara asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mara asilimia 15.
Waziri Mhagama ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kununua viuadudu vya kibaolojia kutoka kwenye kiwanda Tanzania Biotech Products Ltd kilichopo Kibaha mkoani Pwani ili kutekeleza afua za unyunyiziaji viadudu kwenye Halmashauri 184 nchini