MAANDALIZI YA MPANGO MKAKATI WA MALARIA WA MWAKA 2026-2030 YAENDELEA MKOANI DAR ES SALAAM
Posted on: February 25th, 2026Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanafanya kikao kazi muhimu cha mapitio na uandaaji wa Mpango Mkakati mpya wa Malaria wa mwaka 2026–2030 kinacholenga kuweka mikakati madhubuti itakayoongeza kasi ya mapambano dhidi ya malaria katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Kikao kazi hiki kinafanyika Mkoani Dar es Salaam kuanzia tarehe 23 Februari 2026.
Dhamira kuu ya Mpango Mkakati huo ni kuhakikisha kuwa Watu wote Tanzania wanapata huduma za kinga na tiba dhidi ya malaria zilizo endelevu, zenye ubora wa hali ya juu, salama, zenye ufanisi na nafuu. Aidha mpango mkakati huu unalenga katika kuelekea kwenye kutokomeza malaria nchini kwa kuzidi kuongeza Halmashaauri zenye kiwango cha chini cha maambukizi ya malaria kutoka asilimia 50 za sasa hadi kufikia zaidi ya asilimia 80 kwa mwaka 2030.
Mikakati mikuu katika Mpango Mkakati huu ni pamoja na uimarishaji wa Kinga dhidi ya malaria, Uchunguzi na Matibabu sahihi ya Malaria pamoja na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathimini na matumizi ya takwimu ili isaidie katika kufanya maamuzi yenye ushahidi wa kitakwimu, ikienda sambamba na mikakati shirikishi kwa upande wa uagizaji na upatikanaji wa bidhaa na vifaa tiba vya malaria, uelimishaji, uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii pamoja na usimamizi wa mpango.
Mpango mkakati huu utaweka mkazo katika Masuala ya usawa katika upatikanaji wa huduma za malaria ikiwemo usawa wa kijinsia, na mahitaji ya makundi maalumu. Aidha, Mpango Mkakati huu mpya unatarajiwa kuleta tija zaidi katika mapambano dhidi ya malaria hapa nchini, kuelekea katika kutokomeza ugonjwa huu.