Girl in a jacket

MINISTRY OF HEALTH

National Malaria Control Programme (NMCP)

Girl in a jacket

MAFUNZO ELEKEZI KWA WATENDAJI WATAKAOSIMAMIA UTEKELEZAJI WA AFUA YA UPULIZIAJI VIUATILIFU UKOKO YAFANYIKA ARUSHA

Posted on: July 1st, 2026

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM – TAMISEMI) wameanza mafunzo elekezi kwa Waratibu ngazi za Mikoa na Halmashauri watakaosimamia utekelezaji wa afua ya upuliziaji viuatilifu ukoko ndani ya nyumba (Indoor Residual Spraying - IRS) katika Halmashauri zinazotekeleza afua za kutokomeza malaria (Malaria Eimination).


Mafunzo hayo yanafanyika mkoani Arusha na  yanawahusisha waratibu kutoka mikoa na wilaya za Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambapo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kitaalamu na kiutendaji ili kuhakikisha afua hiyo inatekelezwa kwa ufanisi, usalama na kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa kuweza kuleta matokeo yanayokusudiwa..


Afua hii itatekelezwa kwenye vijiji 49 vilivyopo kwenye Halmashauri 12 za Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambayo bado maambukizi ya malaria yanaendelea. Vijiji hivyo vimechaguliwa baada ya ufuatiliaji kubaini uwepo wa wanakaya wenye vimelea vya malaria na kuthibitika kwamba wanakaya hao wamepata maambukizi ya malaria kutoka kwenye maeneo hayo, hali inayoweza kusababisha kuendelea kwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwenye maeneo mengine ya halmashauri hizo ambazo zimelengwa katika kutokomeza malaria. Kupitia utekelezaji wa afua hii, Serikali inalenga kuzuia kuibuka upya (resurgence) kwa ugonjwa wa malaria katika maeneo mengine ya halmashauri ambapo hakuna wagonjwa wa malaria.

Akizungumza katika mafunzo hayo, mkuu wa kitengo cha udhibiti wadudu dhurifu kutoka NMCP Bwana Charles Dismas Mwalimu alisema kuwa maandalizi madhubuti na usimamizi bora wa utekelezaji wa afua hii ni nguzo muhimu katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa katika kuharakisha jitihada za kutokomeza malaria kwenye halmashauri hizo.

Alibainisha kuwa zoezi hili, linaahusisha kupulizia viuatilifu ukoko kwenye kuta na dari za ndani ya nyumba kudhibiti mbu waenezao malaria ambao hupendelea kupumzika maeneo hayo baada ya kufyonza damu. Afua hii ni miongoni mwa afua zenye ushahidi wa kisayansi katika kudhibiti mbu na kukatiza mzunguko wa vimelea wa malaria kwenye mwili wa mbu.

Bwana Mwalimu aliongeza kuwa mafanikio ya afua hii yanategemea maandalizi bora, usimamizi madhubuti na ushirikiano wa karibu kati ya watendaji wa Mikoa, Halmashauri, viongozi wa jamii na wananchi. Tunatarajia washiriki wa mafunzo haya watakwenda kusimamia utekelezaji wa afua hii kwa weledi na kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa kuruhusu nyumba zao kupuliziwa viuatilifu ili kulinda afya zao na kuzuia kuibuka upya kwa ugonjwa wa malaria

Serikali, kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, itaendelea kuimarisha utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti na kutokomeza malaria ili kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa huu nchini ifikapo 2030.

“Ziro malaria inaanza na Mimi, inaanza na wewe inaanza na sisi sote”


}