Girl in a jacket

MINISTRY OF HEALTH

National Malaria Control Programme (NMCP)

Girl in a jacket

MAFUNZO KWA WAPULIZIAJI WA VIUATILIFU UKOKO YAFANYIKA KILIMANJARO

Posted on: August 20th, 2026

Kilimanjaro, Agosti 19, 2026 

Mafunzo kwa wapuliziaji wa viuatilifu ukoko (Sprayer Operators) yamefanyika katika Wilaya za Hai, Moshi Vijijini, Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa afua ya Upuliziaji wa Viuatilifu Ukoko katika kuta ndani ya nyumba, unaolenga maeneo mahsusi (Focal IRS) yaliyochaguliwa.

Mafunzo hayo yameendeshwa na timu za waratibu wa wilaya husika  ambao awali walipatiwa mafunzo maalum kuhusu namna ya kupanga, kusimamia na kutekeleza afua ya Focal IRS katika maeneo yaliyoonekana kuwa na maambukizi ya malaria katika mkoa huo.

Afua ya Focal IRS ni miongoni mwa hatua zinazotekelezwa katika mikoa yenye kiwango cha chini sana cha malaria, hususani Arusha, Kilimanjaro na Manyara, kwa lengo la kuchangia kutokomeza kabisa malaria na kuzuia ugonjwa huo kuenea tena katika maeneo ambayo yamepiga hatua kubwa katika kupunguza maambukizi ya malaria.

Mafunzo hayo yamefanyika chini ya usimamizi wa timu kutoka Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), kwa kushirikiana na timu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, zinazoratibu utekelezaji wa afua hiyo katika mikoa husika.

Katika mafunzo hayo, wapuliziaji wamejengewa uwezo kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya upuliziaji, namna ya kuchanganya na kutumia viuatilifu kwa usalama, pamoja na kuzingatia taratibu na miongozo ya utekelezaji.

Utekelezaji wa zoezi la Focal IRS katika Wilaya za Hai, Moshi Vijijini, Mwanga na Same unatarajiwa kufanyika tarehe 21 na 22 Agosti 2026, katika maeneo yaliyolengwa kutokana na uwepo wa maambukizi ya malaria.

Sambamba na mafunzo hayo, vifaa vya kazi pamoja na viuatilifu vimesambazwa katika wilaya hizo ili kuwezesha utekelezaji wa zoezi hilo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Afua hii ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kulinda mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza malaria na kuhakikisha kuwa maeneo yenye kiwango kidogo cha malaria yanaendelea kuwa salama dhidi ya kuibuka na kuenea tena kwa ugonjwa wa malaria.

“Malaria inatokomezwa na Sisi, Wekeza, chukua hatua, Zero malaria inaanza na Mimi”

}