MAFUNZO YA AFUA YA UNYUNYIZIAJI VIUADUDU VYA KIBAIOLOJIA KWA WATAALAM WA AFYA NGAZI YA MKOA NA HALMASHAURI (MIKOA YA DODOMA NA SINGIDA)
Posted on: February 6th, 2026Leo tarehe 06 Februari, 2026, timu ya kudhibiti wadudu dhurifu kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Taasisi ya utafiti wa Afya Ifakara ( IHI), pamoja na wadau kutoka SWISS TPH – TEMT, wameendelea kutekeleza mafunzo ya kitaalam kuhusu utambuzi wa mazalia ya mbu na matumizi ya viuadudu vya kibaiolojia katika kudhibiti mazalia hayo kwa watalaam wa Afya kutoka katika Halimashauri na Mikoa ya Singida na Dodoma .
Mafunzo hayo yanafanyika Manispaa ya Singida kata ya Mandewa mtaa wa Mandewa yalipo mazalia ya mbu, yakilenga kuongeza ujuzi na uwezo kwa wataalam wa afya waliohudhuria mafunzo hayo katika kutambua aina ya viluilui wa mbu, aina ya viuadudu vya kibaiolojia vinavyotumika kuwaangamiza viluilui hao pamoja na matumizi sahihi na rafiki kwa mazingira katika udhibiti wa mazalia ya mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria.

Aidha watalaam hao wamefundishwa jinsi ya kupima kiwango cha viuadudu vya kibailojia kinachotakiwa kuwekwa kwenye kila zalia kutokana na ukubwa wa zalia, pamoja na kufanya taathimini na ufuatiliaji wa ufanisi wa viuadudu vilivyowekwa kwenye mazalia hayo.
Mafunzo hayo yanawahusisha waratibu wa malaria wa mikoa na halmashauri, maafisa wa udhibiti wa taka ngumu, waratibu wa elimu ya afya kwa umma, wataalam wa udhibiti wa mazalia ya mbu (vector control persons), pamoja na maafisa wa udhibiti wa taka ngumu kutoka kila Halmashauri katika Mikoa hiyo.
Utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji wa viua-dudu katika mazalia ya mbu inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti na kupunguza idadi ya mbu wapevu wanaoeneza ugonjwa wa malaria na kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini, hatua ambayo inachangia kufikia azma ya kitaifa ya kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo mwaka 2030 na kuchangia katika kuboresha afya ya jamii na ustawi wa taifa kwa ujumla.
Viuadudu vya kiabilojia-salama kwa mazingira, hatari kwa viluilui wa mbu!!
“Ziro malaria inaanza na Mimi, inaanza na wewe inaanza na sisi sote”