Girl in a jacket

MINISTRY OF HEALTH

National Malaria Control Programme (NMCP)

Girl in a jacket

MGANGA MKUU WA MKOA WA MBEYA DKT. ELIZABETH NYEME AHIMIZA WASHIRIKI WA MAFUNZO YA UNYUNYIZIAJI WA VIUADUDU VYA KIBAIOLOJIA KUHAKIKISHA AFUA HII INAFANIKIWA KATIKA HALIMASHAURI ZAO

Posted on: March 18th, 2026

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt Elizabeth Nyeme, amewahimiza washiriki wa mafunzo ya utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kuhakikisha wanatumia kikamilifu ujuzi watakaoupata ili kufanikisha mapambano dhidi ya mbu waenezao malaria katika maeneo yao.

Dkt. Nyeme ameyasema hayo leo tarehe 18 Machi, 2026 wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo ya unyunyuziaji wa viuadudu vya kiabailojia katika mazalia ya mbu kinachofanyika mkoani Mbeya.

Mafunzo hayo yanawakutanisha wataalam wa afya kutoka ngazi ya mkoa na Halmashauri kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe, yakilenga kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa afua ya kudhibiti viluilui vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibaiolojia. Mafunzo yanajumuisha vipengele vya nadharia na vitendo ili kuhakikisha washiriki wanapata uelewa wa kina na ujuzi wa moja kwa moja

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Nyeme alisisitiza umuhimu wa washiriki kuandaa mipango kazi yenye uhalisia itakayowezesha utekelezaji madhubuti wa afua hiyo katika maeneo yao. Aidha, aliwataka kuandaa taarifa za utekelezaji na kuziwasilisha kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zao kwa ajili ya maamuzi na ufuatiliaji wa karibu.

Sambamba na hilo, Dkt. Nyeme alizihimiza Halmashauri kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya ununuzi wa viuadudu vya kibaiolojia kwa kutumia mapato ya ndani, ili kuhakikisha uendelevu wa afua hiyo. Pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali waliopo katika maeneo husika ili kuongeza nguvu katika utekelezaji na kufikia matokeo yaliyokusudiwa.

Mafunzo kwa vitendo yamefanyika mjini Mbeya katika eneo la kata ya Ilemi mtaa wa ulambya ambapo washiriki wamepata ujuzi wa kutambua viluilui, kupima ukubwa wa mazalia, pamoja na kuweka kiwango sahihi cha viuadudu na kufanya ufuatiliaji wa ufanisi wake.

Afua ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia inaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kupunguza mazalia ya mbu, kudhibiti ongezeko la mbu wapevu na hatimaye kupunguza maambukizi ya malaria katika jamii kuelekea katika Kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini ifikapo 2030

Kwa pamoja tunaweza kutokomeza malaria.

“Ziro malaria inaanza na mimi, inaanza na wewe, inaanza na sisi sote.”


}