MKUU WA MKOA WA MOROGORO MHE: ADAM KIGHOMA MALIMA AZINDUA RASIMI KAMPENI YA UGAWAJI WA VYANDARUA MKOANI HUMO
Posted on: January 15th, 2026Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amezindua kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa,vinavyotolewa na Serikali ya Tanzania bila malipo kwa wananchi. Uzinduzi huo umefanyika Januari 7, 2025 mkoani Morogoro kwenye kikao cha uhamasishaji kwa viongozi kuhusu mpango wa ugawaji wa vyandarua vyenye Dawa ngazi ya kaya.

Akiongea katika uzinduzi huo, Mhe: Malima amewataka watendaji na wenyeviti wa mitaa na vijiji katika wilaya zitakazohusika kwenye kampeni hii kuhakikisha wanakusanya taarifa zinazotakiwa za wananchi katika maeneo yao kwa ufanisi ili kuhakikisha kuwa kila wanaostahili kupata vyandarua wanapata vyandarua hivyo.
Aidha, Mhe. Malima pia amewataka wananchi wa mkoa wa Morogoro hususani wananchi wa Halmashauri saba zitakazogawiwa vyandarua, kuvitumia vyandarua hivyo ipasavyo ili kuweza kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Malaria unaoenezwa na mbu. “Ni umuhimu wa kila mwananchi kutumia chandarua kwa ajili ya kujikinga na mbu badala ya kutumia vyandarua hivyo kwa shughuli nyingine ambazo siyo lengwa”, Mhe. Malima amesisitiza.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa viongozi wote wa mkoa kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na ugonjwa wa malaria hasa kwenye vikao vyao ngazi ya Mkoa, Halmashauri hadi ngazi ya vijiji.
Mpango wa ugawaji wa vyandarua unahusisha wilaya saba za mkoa wa Morogoro zenye maambukizi makubwa ya Malaria ambazo ni Wilaya ya Mlimba, Kilosa, Malinyi, Morogoro vijijini, Mvomero, Ulanga na Ifakara Mji, ambapo takribani vyandarua 1,474,146 vinategemewa kugawiwa.