Girl in a jacket

MINISTRY OF HEALTH

National Malaria Control Programme (NMCP)

Girl in a jacket

MKUU WA MKOA WA MOROGORO MHE: ADAM KIGHOMA MALIMA AZINDUA RASIMI ZOEZI LA UGAWAJI WA VYANDARUA MKOANI HUMO

Posted on: March 24th, 2026

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye dawa vinavyotolewa na Serikali ya Tanzania bila malipo kwa wananchi kupitia kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kwenye kaya. Uzinduzi huo umefanyika mkoani Morogoro tarehe 23/03/2026

Takribani vyandarua 1,686,333 vinatarajiwa kugawiwa kwa wanakaya 690,632 ambao waliandikishwa katika zoezi la uandikishaji wa kaya lililofanyika katika Halmashauri saba za mkoa wa Morogoro ambazo ni Halmashauri ya Mji Ifakara, Halmashauri ya Mlimba, Mvomero, Morogoro, Malinyi, Kilosa na Ulanga kuanzia mwishoni mwa mwezi Januari, 2026 na kuhitimishwa tarehe 18, Marchi, 2026.

Mhe. Malima amesema kua vyandarua hivyo vitasaidia kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wanajilinda na mbu waenezao ugonjwa wa malaria kwa kuzingatia matumizi sahihi na kuhakikisha kila mwanafamilia analala ndani ya chandarua kila siku ili kuweza kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria na hatimae kuweza kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Mhe: Malima ameipongeza Serikali kwa kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu na uhamasishaji, utunzaji wa mazingira, udhibiti mbu wapevu waenezao Malaria kupitia unyunyuziaji wa viuadudu vya kibaiolojia, ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kupitia huduma za mama na mtoto pamoja na kampeni za ugawaji wa vyandarua kwenye shule za msingi na kwenye kaya na kuweza kupunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022  na kufikia asilimia 5.5 mwaka 2025.

Aidha, Mhe: Malima amewataka wananchi wa mkoa wa Morogoro kutumia vyandarua hivyo vinavyo tarajiwa kugaiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa na Serikali ikiwa ni hatua ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Malaria ili kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

}