TANZANIA YAZINDUA MJADALA KUWEKA VIPAUMBELE UFADHILI WA MFUKO WA DUNIA KUKABILI UKIMWI, KIFUA KIKUU NA MALARIA MZUNGUKO WA NANE (GC8)
Posted on: April 8th, 2026Serikali ya Tanzania imezindua rasmi Mjadala wa Kitaifa (Country Dialogue) wa siku mbili kwa ajili ya kuandaa andiko la kuomba fedha kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria Mzuko wa nane (Grant Cycle 8 - GC8).
Hatua hii inalenga kuhakikisha wadau wote wanafanya mjadala na kuja na vipaumbele vitakavyozingatiwa katika andiko la kuomba fedha kupitia ufadhili huo kwa ajili ya mapambano ya magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kwa kipindi cha utekelezaji cha kuanzia Januari Mosi, 2027 hadi Desemba 31, 2029.
Akifungua kikao cha siku mbili Aprili 8, 2026 Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema tukio hilo ni fursa muhimu ya kuonyesha vipaumbele vya kitaifa vinavyotokana na mjadala baina ya Serikali, Wadau wa Maendeleo,Watekelezaji, jamii na wadau wote.
"Ushirikiano huu unaonyesha dhamira thabiti ya kusikiliza sauti zote na kuhakikisha maamuzi yanayofanywa yanaleta faida kwa nchi," amesema Dkt. Shekalaghe.
Amefafanua kuwa, katika wiki mbili zilizopita, zaidi ya wawakilishi 130 wa mashirika yasiyo ya kiserikali walikutana kujadili vipaumbele vya jamii, makundi muhimu, na mifumo ya jamii. Pia, zaidi ya wawakilishi 120 wa serikali kutoka mikoa mbalimbali walishiriki kikao cha kuainisha vipaumbele vya kitaifa kulingana na sera, ushahidi wa kisayansi na hali halisi za programu.
Dkt. Shekalaghe amesema huu si mkutano wa kawaida, bali ni juhudi za kimkakati zisizo na upendeleo ili kuhakikisha hakuna sauti inayoachwa nyuma.
Tanzania imepatiwa takriban USD 538.6 milioni kwa kipindi cha 2027–2029 kufanikisha programu za HIV, TB na malaria. Hii ni fursa ya kipekee ya kuharakisha maendeleo na kuziba mapengo muhimu kwenye huduma za afya, lakini pia ni wajibu wa kuhakikisha kila dola inatumika kwa mikakati yenye tija, uwazi, na matokeo kwa wananchi.
Mjadala huu kuelekea kuandaa andiko la GC8 unalenga kufikia mabadiliko makubwa katika usimamizi wa fedha. Umebeba mwelekeo mpya wa kutoka kwenye programu za ugonjwa mmoja hadi mfumo wa afya uliounganishwa, kuweka mkazo kwenye uwekezaji wenye athari kubwa na thamani ya fedha, kuwekeza katika makundi yaliyo hatarini zaidi, kuimarisha ufadhili wa ndani na kuendeleza ubunifu na ustahimilivu wa mifumo ya afya.
Mjadala huu ni jukwaa la kufanya maamuzi muhimu, likilenga kukubaliana vipaumbele vya kitaifa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Taifa, kubaini mapengo katika programu na mahitaji ya fedha, kuweka mkazo wa uwekezaji wenye tija, na kuunganisha vipaumbele vya jamii, serikali na wadau wa kimataifa.
Washiriki wote wametiwa moyo kuzingatia maslahi ya Taifa, uwazi, usawa wa sauti zote, na uwajibikaji, ili matokeo ya mkutano huo yafikie ndoto za mamilioni ya Watanzania.
Dkt. Shekalaghe amesema Tanzania inapaswa kuendeleza uwekezaji wa fedha za ndani, ustahimilivu wa mifumo ya afya, uwezo wa taasisi, kuunganisha programu za magonjwa katika huduma za msingi za afya, na kuimarisha mifumo ya jamii endelevu ikiwa na lengo kuhakikisha kuwa faida za Global Fund zinaendelezwa na kuimarishwa kupitia uwajibikaji wa pamoja.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Shekalaghe amesema Mjadala huu ni fursa ya kihistoria kwa Tanzania. Ubora wa majadiliano, vipaumbele vitakavyopangwa, na mshikamano wa wadau utaamua mafanikio ya maombi ya fedha hizi kwa manufaa ya wananchi.