VIKAO VYA MAANDALIZI YA AWALI VYA KUTATHIMINI NA KUHITIMISHA ZOEZI LA UANDIKISHAJI TAARIFA ZA KAYA KWENYE KAMPENI YA UGAWAJI WA VYANDARUA VINAENDELEA MKOANI MOROGORO
Posted on: March 14th, 2026Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) pamoja na Wadau inatekeleza afua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa Malaria kama vile afua ya udhibiti mbu waenezao Malaria ikiwemo kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bila malipo kwenye kaya. Kampeni hii kwa sasa inaendelea kufanyika Mkoani Morogoro.
Kampeni hii ilianza mwishoni mwa mwezi Januari 2026, kwa kufanya vikao vya uhamasishaji katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri na kufuatiwa na uandikishaji wa taarifa za kaya ambapo kaya zote katika Halmashauri za Wilaya ya Morogogoro, Mvomero, Kilosa, Mlimba, Malinyi, Ulanga pamoja na Halmashauri ya Mji Ifakara ziliandikishwa kupitia watendaji na wenyeviti wa vijiji na mitaa pamoja na wahudumu wengine wa kujitolea
Kwasasa, zoezi hili linaendelea kwa kufanya vikao vya maandalizi ya awali ya kutathimini na kuhitimisha zoezi la undikishaji wa taarifa za kaya mkoani humo vikiwa nalengo la kuendesha majadiliano ya pamoja kati ya Wizara ya Afya (NMCP, Bohari ya Dawa (MSD)), TAMISEMI, ofisi ya Mkuu wa Mkoa, pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Timu za uendeshaji wa shughuli za afya za Wilaya. Majadiliano hayo yamejikita zaidi kwenye upitiaji wa takwimu za uandikishaji wa kaya katika vijiji na mitaa ili kuweza kufanya tathimini na kuhitimisha zoezi hilo ikiwa ni maandalizi ya usambazaji na ugawaji wa vyandarua kwenye kaya.
Vikao hivi vimedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapatiwa vyandarua kulingana na taarifa za uandikishaji wa kaya na hatimaye kusaidia wananchi kuweza kujikinga na ugonjwa wa Malaria na kufikia lengo la kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030.
“Zero Malaria Inaanza na Mimi”