Girl in a jacket

MINISTRY OF HEALTH

National Malaria Control Programme (NMCP)

Girl in a jacket

VIONGOZI WA WILAYA ZA HANDENI NA KILINDI MKOANI TANGA WAHIMIZA USHIRIKIANO WA JAMII KATIKA KUTOKOMEZA MALARIA

Posted on: April 21st, 2026

Wakuu wa Wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga wamezindua kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa katika maeneo yao. Kampeni hiyo inalenga kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini. Wakizungumza katika vikao vya uhamasishaji vilivyofanyika katika Halmashauri za wilaya zao kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za pamoja katika kudhibiti na hatimaye kutokomeza ugonjwa huo.

Wakuu hao wameeleza kuwa malaria bado ni tishio kubwa kwa afya ya wananchi na huathiri kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya taifa, hususan wanawake na watoto, hivyo kuna ulazima wa kuchukua hatua madhubuti na endelevu ili kuilinda jamii. Aidha, wamepongeza juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya - Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kwa kuendelea kuratibu na kusimamia kampeni za kitaifa zinazolenga kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo nchini. Aidha, Viongozi hao walibainisha kuwa ushirikiano wa sekta mbalimbali kama vile Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kutasaidia kuboresha mifumo ya ufuatiliaji, utoaji wa elimu na taarifa, na usimamizi wa takwimu sahihi katika mapambano dhidi ya malaria.

Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa kiwango cha maambukizi ya malaria kwa wanafunzi wa shule za msingi (SMPS) uliofanyika mwaka 2025, hali ya maambukizi katika Mkoa wa Tanga bado inahitaji uangalizi na hatua za ziada. Mkoa kwa ujumla una kiwango cha maambukizi cha takribani asilimia 3.9, huku Halmashauri ya Mji Handeni ikiongoza kwa asilimia 10.5, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni yenye asilimia 8.8, na Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ikiwa na asilimia 1.7

Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa, licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna haja kubwa ya kuimarisha na kuendeleza mikakati madhubuti ya kudhibiti malaria ili kupunguza zaidi maambukizi na kulinda afya ya jamii.

Kutokana na hali hiyo, Wakuu hao wamehimiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kwa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka, pamoja na kuwahusisha viongozi wa Dini na Kimila ili kuongeza ufanisi wa uhamasishaji na  kuhakikisha uadilifu katika zoezi la uandikishaji wa kaya ili vyandarua vitakavyo gawiwa viwafikie walengwa halisi,

Kwa mujibu wa mipango iliyowekwa, kampeni ya ugawaji vyandarua inatarajiwa  kugawa idadi ya vyandarua 63,602 kwa Halmashauri ya Mji wa Handeni na  vyandarua 232,533 ya Halmashauri ya Wiaya ya Kilindi.

 “Tumedhamilia kutokomeza Malaria, Wakati ni sasa, Tunaweza – Ziro Malaria Inaanza na Mimi.”

}