WANAWAKE NI JESHI KUBWA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA MALARIA HAPA NCHINI
Posted on: March 8th, 2025
Wanawake wana jukumu kubwa katika mapambano dhidi ya malaria hapa nchini. Tunapoadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu wa 2025, ni muhimu kwa wanawake wote kuendelea kushiriki kikamilifu katika kutumia afua za malaria ikiwemo kinga dhidi ya malaria, uchunguzi na matibabu sahihi ya malaria pamoja na kukamilisha dozi kulingana na maelekezo ya watoa huduma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria, imeendelea kuboresha huduma za Malaria kwa wanawake hususani pale wanapokuwa wajawazito. Huduma za malaria wakati wa ujauzito zinatolewa bila malipo katika vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za Afya nchini ni kupimwa malaria ili kubaini kama mjamzito ana maambukizi ya malaria, kupata chandarua chenye dawa bila malipo wakati wa hudhurio la kwanza la kliniki, kupata dozi tatu au zaidi za dawa ya SP katika kipindi chote cha ujauzito ili kumkinga mama na mtoto aliye tumboni mwake dhidi ya madhara ya malaria.
Vyandarua vyenye dawa hutolewa bila malipo pia kwa watoto chini ya mwaka mmoja wakati wa chanjo ya surua/rubella. Wajawazito wote wanahimizwa kuanza kliniki mapema pale tu wanapojihisi ni wajawazito ili wapate huduma zote za malaria bila malipo yeyote.
Kuongezeka kwa utumiaji wa huduma hizi kwa wajawazito kumesaidia kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini kutoka 14.8% mwaka 2015 hadi 8.1% mwaka 2022. (Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa viashiria vya malaria mwaka 2022- Malaria Indicator Servey).
Siku hii ya Wanawake duniani 2025, inatukumbusha kuwa wanawake ni jeshi la ushindi katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini. Mwanamke akielewa namna ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria ataleta mabadiliko chanya katika kaya yake na kuhakikisha wanafamilia wote wakiwemo watoto wanakua salama na hivyo kuchangia katika malengo ya kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030
ZIRO MALARIA INAANZA NA MIMI, INAANZA NA WEWE, INAANZA NA SISI SOTE