DKT. SHEKALAGHE AWATAKA WARATIBU WA MALARIA NCHINI KUFANYA KAZI KWA UBUNIFU
Posted on: April 13th, 2023Na WAF – Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amewataka waratibu wa Malaria nchini kuongeza ubunifu na kuweka mikakati itakayosaidia kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini.
Dkt. Shekalaghe amesema hayo leo 24 Machi, 2023 jijini Dodoma wakati akifunga mkutano uliohusisha waganga wakuu wa Mikoa na waratibu wa Malaria kwa ajili ya kupeana miongozo na mikakati itakayosaidia kupunguza na kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria.
Dkt. Shekalaghe amesema ugonjwa wa Malaria bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo nchini hivyo waratibu wanatakiwa kushirikiana na kuweka mikakati madhubuti ambayo kama itatumika vyema itasaidia kutokomeza kabisa ugonjwa huo nchini.
“Ningependa kuona vikao vya ngazi ya Mkoa vinafanyika kila robo au nusu mwaka ili kutathmini utendaji wa uratibu wa Malaria, kujadiliana kwa pamoja ni jambo la msingi litakalosaidia katika mapambano dhidi ya Malaria”. Amesema Dkt. Seif.
Katibu Mkuu huyo amewataka waratibu wa Malaria kutembelea maeneo yenye kesi nyingi na kuchukua takwimu katika vituo vya afya kuanzia ngazi ya Zahanati na kuendelea, ameongeza kuwa changamoto kubwa katika Halmashauri ni ukosefu wa Magari hivyo amewataka kuazima magari ya idara nyingine ili kutekeleza majukumu yao.
Aidha, Dkt. Seif amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia vyema dawa zinazopelekwa katika maeneo yao ili ziweze kukidhi matibabu kwa wagonjwa wanaopatikana. Amesema kuna baadhi ya maeneo dawa zilizopelekwa zinawahi kuisha lakini zinakua haziendani na idadi ya wagonjwa waliotibiwa hali inayopelekea kuwepo hoja namna zinazotumika katika matibabu.
Kikao hiki cha mwaka ni cha kwanza kilichokutanisha kwa pamoja waratibu wa Malaria wa Mikoa na Wilaya nchi nzima ambapo hapo awali waratibu hao walikua wanakutana kulingana na kanda walizopo hali iliyosababisha kutopata uzoefu kutoka kanda zingine.