JAMII YAFANYA UFUATILIAJI WA HUDUMA ZA UGONJWA WA MALARIA
Posted on: May 11th, 2026Wizara ya Afya kupitita Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na wadau SIKIKA na Mtandao wa Jamii wa Kusaidia Kutokomeza Malaria Tanzania – CONAMET inatekeleza shughuli ya kufanya ufuatiliaji wa huduma za malaria kupitia jamii (Community – Led- Monitoring - CLM) ambapo wanajamii wanashiriki kikamilifu katika kukusanya, kuchambua na kutumia taarifa ili kuboresha huduma za malaria.
Ufuatiliaji huo umejikita katika huduma za malaria zinazotolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na jamii ikiwemo elimu na uhamasishaji jamii juu ya ugonjwa wa malaria, matibabu ya malaria ikiwemo vipimo na dawa, tiba kinga ya malaria (SP) kwa wajawazito pamoja na upatikanaji na matumizi ya vyandurua.
Ufuatiliaji huo unasimamiwa na Asasi isiyo ya kiserikali iitwayo Sikika ambayo imepewa fedha kupitia programu ya uimarishaji wa huduma za afya (Resilient and Sustainable Systems for Health -RSSH) kwa ufadhili wa mfuko wa Dunia unaoshughulikia magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.
Ufuatiliaji wa majaribio ulianza mwezi Aprili 2025 na unaendelea kutekelezwa katika mikoa ya Tabora na Katavi, hususan katika Halmashauri za Kaliua, Nzega na Mlele. Katika ufuatiliaji huo, wanajamii wa kujitolea walipatiwa mafunzo kuhusu ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa. Baada ya mafunzo, walikusanya taarifa katika kata 10 za kila Halmashauri na kufanikisha kuwafikia jumla ya wanajamii 300 kwa kila Halmashauri inayotekeleza ufuatiliaji huo. Aidha, taarifa zilizokusanywa zilichambuliwa na mrejesho kutolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo watoa huduma za afya, wanajamii pamoja na viongozi wa vijiji na mitaa walishiriki katika mijadala na kuandaa mipango kazi ya kukabiliana na changamoto zilizobainishwa na wanajamii.
Ufuatiliaji huo unakusudia kupata mrejesho kutoka kwa wanajamii kuhusu huduma zinazotolewa, pamoja na kubaini changamoto zinazojitokeza katika upatikanaji wa huduma za malaria. Kupitia mchakato huo, wadau hushirikiana na wanajamii kujadili namna ya kukabiliana na changamoto zilizobainishwa na kutoa ushauri kwa mamlaka husika ili kuchukua hatua stahiki za kuboresha huduma hizo, kwa lengo la kuimarisha juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.