Girl in a jacket

MINISTRY OF HEALTH

National Malaria Control Programme (NMCP)

Girl in a jacket

VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA WAHIMIZWA KUSIMAMIA USAFI WA MAZINGIRA ILI KUANGAMIZA MAZALIA YA MBU NDANI YA JAMII

Posted on: November 30th, 2022

Viongozi wa Serikali za Mitaa nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira kwenye maeneo yao pamoja na kufukia madimbwi yote ili kuteketeza mazalia ya mbu yanayopelekea kuongezeka kwa mbu na ugonjwa wa malaria nchini.

Hayo yamesemwa leo Jijini Tanga na Waziri wa Afya Mhe. Ummy wakati akizindua Afua ya unyunyiziaji wa viuadudu vya Kibaiolojia kwenye mazalia ya Mbu kwa Wilaya za Tanga, Handeni na Lushoto iliyofadhiliwa na Serikali ya Uswisi kupiti Shirika la Maendeleo la Uswisi.

Amesema licha ya kutekeleza afua hiyo ya unyunyiziaji wa viuwadudu vya kibailojia kwenye mazalia ya mbu bado pia Jamii inahitajika kuboresha usafi wa mazingira kwa kuangamiza mazalia yote ya mbu katika maeneo tunayoishi hivyo basi Viongozi wa Serikali za Mitaa wawajibike katika kuhimiza usafi wa mazingira.

“Tukifunika madimbwi itasaidia kuzuia magonjwa yaenezwayo na mbu pamoja na magonjwa mengine kama Dengue,matende na mabusha homa ya bonde la ufa na Chikungunya” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Hata hivyo Waziri Ummy ametaka kutekelezwa kwa usimamizi wa Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009 na Sheria ya Usimamizi ya Mazingira ya mwaka 2004.

Amesema hatua hiyo ikifanyika kikamilifu, itasaidia kupunguza idadi ya mazalia,kupunguza wingi wa mbu katika maeneo tunayoishi na hatimaye kupunguza maambukizo ya ugonjwa wa Malaria na magonjwa mengine.

"Yeyote ambaye hatotekeleza wajibu wake katika kuharibu mazalia ya mbu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria hizi" amesisitiza Waziri Ummy.

"Ugonjwa wa Malaria bado ni tatizo katika nchi yetu, hata hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria nchini kati ya watu 100 wanaofika hospitali 10 wana changamoto ya Malaria"Amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.

Aidha,Waziri Ummy amesema mradi huo ambao utakuwa wa miaka miwili utaweza kuleta manufaa yaliyokusudiwa na hivyo kuendelea na afua zingine za udhibiti wa Malaria ikiwemo ya kuwa na mazingira safi.

}